Saturday, 21 December 2013

WATANI KUAMUA NANI JEMBE TAIFA LEO

Mashabiki wa timu ya Yanga Fc.
Mashabiki wa timu ya Simba Fc.

WATANI wa jadi katika soka
nchini, timu za Yanga na Simba,
leo zinashuka katika Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam
kuhitimisha majigambo ya ‘Nani
Mtani Jembe’ baina yao katika
mechi kali inayofanyika chini ya
uratibu wa mdhamini wao,
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Mbali ya wapenzi na mashabiki wa
timu hizo kusubiri kuona ‘nani
mtani jembe’ kati yao, pia
watapata fursa ya kushuhudia
nyota wapya waliosajiliwa kupitia
dirisha dogo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam
jana, Kaimu Katibu Mkuu na Ofisa
Habari wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Boniface
Wambura, alisema maandalizi ya
mechi hiyo ya aina yake
yamekamilika.
Wambura alisema vikosi vya ulinzi
na usalama katika mechi ya leo
vimekamilika kila idara na
kwamba Barabara ya Taifa
inayoanzia Keko-Maghorofani hadi
Barabara ya Mandela, itafungwa
kuanzia saa 12 asubuhi kupisha
hekaheka za mtifuano huo.
Alisema magari hayataruhusiwa
kuegeshwa kuanzia eneo la Baa ya
Minazini hadi msikiti
unaotazamana na Uwanja wa
Uhuru, hivyo magari yote
yataegeshwa nje ya Uwanja wa
Ndani wa Taifa – kando ya
Barabara ya Mandela.
“Magari yatakayoruhusiwa kuingia
maeneo hayo na hata ndani ya
Uwanja wa Taifa ni yatakayokuwa
na stika zilizotolewa na TFF.
Tunawaomba wadau na mashabiki
wa soka kuheshimu na kutii
maagizo ya vikosi vya ulinzi,”
alisema Wambura.
Aliongeza kuwa milango ya
kuingilia uwanjani itakuwa wazi
kuanzia saa sita mchana ambapo
baada ya mauzo ya tiketi ya jana,
zoezi hilo litaendelea leo nje ya
uwanja huo kabla ya mechi ili
kuwapa mashabiki fursa ya kukata
na kuingia moja kwa moja.
Pambano la leo linasubiriwa kwa
hamu na mashabiki wa soka
wanaohitaji sio tu kuona nyota
wapya waliosajiliwa na klabu hizo,
pia kujua ‘nani jembe’ ndani ya
uwanja kwani kwa nje ya uwanja,
Yanga ni kama imeshinda
kutokana na kuwa kwenye
mazingira mazuri kisaikolojia.
Nje ya uwanja, Nani Mtani Jembe
ilihusisha vita baina ya mashabiki
wa kila klabu ‘kupora’ mamilioni
ya mwingine kupitia shindano la
kinywaji cha Kilimanjaro Premium
Lager ambapo Simba ilizidiwa na
Yanga kwa kiasi kikubwa cha pesa.
Ukiondoa shangwe ya mashabiki
wa Yanga kumpata mshambuliaji
wa kimataifa wa Uganda,
Emmanuel Okwi akitokea SC Villa
ya Uganda na Juma Kaseja, Simba
leo itakuwa na makipa waliowahi
kudaka Jangwani kwa vipindi
tofauti, Ivo Mapunda na Yaw
Berko.
Nyuma ya majina hayo makubwa,
Yanga ilinasa saini ya kiungo
Hassan Dilunga kutoka Ruvu
Shooting ya Pwani, wakati Simba
iliwasainisha kwa mpigo kiungo
mchezeshaji Awadh Juma Issa
kutoka Mtibwa Sugar ya
Morogoro na Ally Badru Ally
kutoka Canal Suez ya Misri.
Kila timu ilishajichimbia kambini
kunoa makucha kuelekea
pambano hilo ili kusawazisha
makosa yaliyowafanya watani hao
kutoka sare ya 3-3 katika mechi
ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu
Bara iliyochezwa Oktoba 20.
Uwepo wa nyota wapya kwa kila
upande ambao watashirikiana na
wakali wengine, unalifanya
pambano la leo liwe lenye mvuto
wa aina yake ambapo kiingilio cha
chini ni sh 5,000 kwa viti vya
kijani.
Kwa upande wa viti vya rangi ya
bluu, kiingilio ni sh 7,000; viti
vya rangi ya chungwa sh 10,000;
VIP C ni sh 15,000; VIP B sh
20,000 huku VIP A sh 40,000.
Kwa upande wa waamuzi, kati
atasimama Ramadhan Ibada ‘Kibo’
wa Zanzibar, atakayesaidiwa na
Ferdinand Chacha wa Bukoba na
Simon Charles wa Dodoma huku
Israel Nkongo wa Dar es Salaam
akiwa mezani. Kazi ya kutathimini
utendaji wa waamuzi wote
itakuwa chini ya Soud Abdi wa
Arusha.
MECHI TANGU 2010
Rekodi ya watani hawa
inaonyesha kuwa mechi ya leo ni
ya tisa tangu mwaka 2010 na
katika mechi nane, Yanga
imeshinda tatu, Simba mbili na
wamekwenda sare tatu.
Aprili 18, 2010: Simba 4, Yanga 3
Oktoba 16, 2010: Yanga 1, Simba
0
Machi 5, 2011: Yanga 1, Simba 1
Oktoba 29, 2011: Yanga 1, Simba
0
Mei 6, 2012: Simba 5, Yanga 0
Oktoba 3, 2012: Yanga 1, Simba 1
Mei 18, 2013: Yanga 2, Simba 0
Oktoba 20, 2013: Simba 3, Yanga
3


posted by kulwa ngatigwa

No comments:

Post a Comment