MWENYEKITI wa Klabu ya
Yanga, Yusuf Manji,
ametangaza rasmi kutowania
tena nafasi ya uenyekiti
kwenye uchaguzi mkuu wa
klabu hiyo utakaotangazwa
baadaye mwakani.
Manji alichukua wadhifa huo
mwaka jana baada ya
kuondolewa kwa aliyekuwa
Mwenyekiti, Lloyd Nchunga,
aliyekuwa amebakiza miaka
miwili ya uongozi wake
klabuni hapo .
Manji ambaye pia ni mfadhili
wa klabu hiyo alitoa tamko juu
ya nia yake hiyo jana kwenye
makao makuu ya klabu hiyo
yaliyopo Jangwani, Kariakoo
jijini Dar es Salaam huku
akitoa sababu kuwa ni
kuwapisha wengine wenye
uwezo wa kuiongoza timu hiyo
nao kuchukua jahazi.
Amesema ametangaza
kutowania nafasi hiyo mapema
ili kuwapa nafasi nzuri
wanaotaka kufanya hivyo
wajipange mapema .
“Sitagombea tena uenyekiti
kwenye uchaguzi ujao,
nitawaachia wengine
waendeleze hapa nilipoishia
mimi , nimetangaza mapema ili
wanaoitaka hii nafasi
wajipange, maana wapo wenye
nia lakini wanahofia kuchuana
na mimi .
“Ninaweza kugombea lakini si
sasa labda baadaye na siyo
uchaguzi huu, nitafikiria
kwanza kabla ya maamuzi
hayo, ” alisema Manji .
Kiongozi huyo aliongeza kuwa
ataendelea kuiongoza Yanga
kwa miezi saba iliyosalia.
Aidha, alisema kuwa bado
tarehe rasmi ya uchaguzi huo
haijafahamika na kudai kuwa
itajulikana mara baada ya
Mkutano Mkuu wa Yanga
utakaofanyika Januari 19 ,
mwakani.
“Nikishajitoa rasmi kwenye
madaraka ya uongozi wa Yanga
baada ya kuwa nimemaliza
muda wangu nitaendelea kuwa
shabiki wa kawaida wa Yanga
kama ilivyo kwa wengine na
kuhusu udhamini litabaki kuwa
suala la klabu kuchagua
mdhamini wao,” alisema
Manji.
posted by kulwa ngatigwa
No comments:
Post a Comment